KIJANA AU BINTI USIJIDANGANYE KWENYE NDOA HUTAISHI NA UMBILE WALA FEDHA
…UTAIINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI… (Isaya 58:12)
Mafundisho ya Neno la Mungu
Na: Isaac Mwanzalila
Upande wa pili wadada wengi licha ya kujali pia suala la muonekano wa nje, wao huangalia zaidi uwezo wa mtu kifedha na baadhi yao kitaaluma pia. Hii ni kwa sababu wanawake wengi wanaamini katika kupata matunzo mazuri wawapo kwenye ndoa zao. Hivyo kupata mwenza ambaye ataweza kumtunza na kumjali kwa mambo mbalimbali ya maisha ikiwa ni pamoja na mavazi, makazi mazuri, usaifiri, nk ni moja ya kipaumbele kwake, naam sijasema wote bali wengi kwa kila upande.
Mitazamo ya makundi haya mawili hapo juu nimeithibitisha kufuatia majadiliano, maswali na semina za kiroho ninazofanya na wahusika. Kimsingi vipo vigezo vingine ambayo kila upande huzingatia lakini hivi nilivyotaja ndio vikubwa kwa wengi hata kama hawatasema moja kwa moja kwako, ila kwetu watumishi wanasema, naam vijana wa kiume husema Mtumishi ‘figure ina matter’ na wadada husema ‘uhakika wa matunzo mazuri una matter’.
Ukweli ni kwamba hii ni mitazamo ambayo imegharimu na inaendelea kugharimu wanandoa wengi sana. Walioko nje ya ndoa hawajui athari zake na walioko kwenye ndoa hawataki kusema maana wanahofia kupata aibu mbele ya jamii licha ya kupitia kwenye maumivu ambayo ni siri yao ingawa kila mmoja amempata yule ambaye alimtaka.
Ukisoma Biblia katika 1Samweli 16:1-13 utaona habari ya Nabii Samweli kwenda kwenye nyumba ya Yese ili kumtia mmoja wa watoto wake mafuta kuwa mfalme wa Israeli kufuatia uasi wa mfalme Sauli. Ndani ya habari hii kuna mafunzo muhimu yanayohusu namna ya kufanya maamuzi katika maisha. Hivyo nimeona vema kuitumia katika kufafanua somo hili kwani inauhusiano mkubwa sana na uamuzi wa kutafuta mwenza wa maisha.
Biblia katika 1Samweli 16:6-7 inasema ‘Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake. Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo’.
Tunaona kwamba Mungu hakuwa amemtajia Samweli jina la mtoto ambaye alipaswa kumtia mafuta ila alimwambia ‘nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako’. Hivyo Samweli alipofika alimwagiza Yese kuwaleta watoto wake wote na kuanza kuwapitisha mbele zake, akisubiri maelekezo ya BWANA kuhusu aliyekusudiwa.
Mtoto wa kwanza wa Yese aliyeitwa Eliabu ndiye alianza, kijana huyu alipopita, Samweli akasema huenda huyu ndiye napaswa kumtia mafuta. Kufuatia wazo hilo, BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi NIMEMKATAA. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo’.
Habari hii inatufanya tuelewe kwamba wazo na uamuzi wa Samweli wa kutaka kumtia mafuta Eliabu ulitokana na mwonekano wa nje wa kijana yule kwa maana ya urefu, uzuri wa sura na umbile lake. Jambo hili linatufundisha kwamba kumbe nyuma ya sura ya mtu, umbile lake au mwonekano wake wa nje kuna nguvu au sauti inayoweza kuongoza maamuzi ya mtu au watu wengine, na hivyo ni heri kuwa makini tusiingie kwenye metego huo.
Hivyo kutokea kwenye habari hii yafuatayo ni mambo muhimu kuyajua na kuyazingatia katika suala zima la kutafuta mwenza wa maisha:
Usitumie mwonekano wa nje wa mtu (sura yake, kimo au umbile lake) kama kigezo kikuu cha kumchagua au kumkubali awe mwenza wako. Naam uso wake sio moyo wake, kwa sura ya nje anaweza kuwa kondoo lakini kwa sura ya ndani (moyoni) ni mbwa mwitu. Naam ndioa maana imeandikwa ‘Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa’ (Mithali 31:30).
Umbile la mwenza wako halitakufanya uache kitanda chako na kulala chini, chumba kingine au hata nje ya nyumba, bali tabia ya mwenza wako inaweza kukupelekea kufanya hayo. Naam umbile la mwenza halitakufanya ufikie mahali pa kujutia ndoa yako bali tabia yake inaweza kukupelekea kufanya hayo.
Jifunze kumuuliza Mungu, huyu niliyemwona ambaye ninakusudia aje kuwa mke au mume wangu, je nimeona sawasawa na mapenzi yako kwangu au la? Maana wewe umesema ‘Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo’, naam nakuomba unipe macho ya kiroho nione sawasawa.
Usitumie mazingira ya nje ya mtu (fedha, mali au elimu) kama kigezo kikuu cha kumchagua au kumkubali awe mwenza wako wa maisha. Naam anaweza kuwa na elimu nzuri, fedha ya kutosha na mali nyingi lakini moyoni mwake hakuna upendo au hofu ya Mungu. Mali na yote yanayofanana na hayo ni vitu mnavyoweza kuvitafuta na kuvipata kwa pamoja ikiwa ndoa yenu ina amani na upendo wa kweli. Kumbuka amani ya kweli haitokani na wingi wa mali alizonazo mtu bali mahusaiano mazuri kati yenu
Usiingie kwenye ndoa kama vile maonyesho au kwa kusikiliza watu wanasema nini, kumbuka ndoa ni ya watu wawili, naam ni wewe ndiye utakayekutana na mateso au raha na si wao. Hivyo pale unapopewa ushauri kuhusu kuoa au kuolewa rudi kwenye Biblia uone neno la Mungu linasemaje juu ya wazo hilo na zaidi mwombe Mungu akuongezee utayari wa kutii mapenzi yake kwenye maisha yako.
Biblia inaeleza wazi kwamba wapo watu wazuri kwa sura na maumbile, hivyo siyo kosa kuwa na mwenza wa aina hiyo na ukifanikiwa kumpata aliyetulia hongera sana. Hata hivyo ni muhimu utambue sio wewe peke yako unayemuona ni mzuri, mpo wengi. Mbaya zaidi ni endapo mwenza wako atakuwa na tabia ya kujiona au kujisika kweli yeye ni mzuri hususani kufuatia sifa anazopewa na watu wa nje. Hivyo ni muhimu ujifunze namna ya kuomba na kuishi na mtu wa aina hiyo, vinginevyo ndoa yako haiwezi kuwa na utulivu.
Hakika ni rahisi kumpenda mtu Kwa kuangalia sura yake, umbile lake au uwezo wake, bali wewe, hakikisha kabla hujaamua kuishi naye unatafuta kujua ikiwa ni wa mapenzi ya Mungu kwako au la.
Mpenzi msomaji, kwenye ndoa hutaishi na umbile wala sura ya mtu pekee, bali zaidi tabia ya mwenza wako, naam tabia ndiyo inayoamua aina ya maisha ya ndoa yako yatakavyokuwa. Tabia ya mtu ndiyo inayopelekea wanandoa kulala vyumba tofauti ndani ya nyumba moja, au mmoja kulala chini na mwingine kitandani ndani ya chumba kimoja, tabia ndiyo inayopelekea wanandoa kupigana ilihali wameokoka nk.
Hii ni kwa sababu maisha ya mtu yamefichwa ndani ya moyo wake na si umbile lake wala sura yake wala mali zake. Kumbuka imeandikwa ‘Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? (Yeremia 17:9). Naam huwezi kumjua mtu kwa kumwangalia kwa nje ndiyo maana unahitaji kumhusisha Mungu anayeona sura ya ndani (moyo wa mtu) akusaidie.
Naam kwa kalamu ya mwandishi, nakuhimiza, mpe Mungu nafasi akusaidie na kukuongoza kupata mwenza sahihi wa maisha na si kuangalia umbile la mtu, uzuri wa sura yake, uwezo wake kifedha au kielimu kama vigezo vikuu vya kufanya maamuzi. Siandiki masomo haya kwa sababu naweza kuandika, bali naandika kwa sababu nimeagizwa kuandika ili kuwaepusha wengi na kile ambacho Mtume Paulo alikiita ‘shida iliyopo kwenye ndoa’ na zaidi ili kuwasaidia wengi kulitumikia ipsasvyo kusudi la Mungu kwenye maisha yao, kupitia ndoa zao (asomaye na fahamu).
Utukufu na Heshima vina wewe Yesu, Wastahili BWANA wangu.
![]() |
Ev.Isaac Mwanzalila |
Vijana tujifunze kutoka Kwa hili somo
ReplyDeleteVery powerful
ReplyDelete