SHULE YA MUNGU MAISHANI MWAKO.
... UTAINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI...(ISAYA 58:12)
Na: Isaac Mwanzalila
KWELI_KUU: Maisha ni uanafunzi katika kujifunza kumjua Mungu kwa kumjua Kristo Yesu Bwana.
Zaburi 32:8
Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, Nitakushauri, jicho langu likikutazama
UTANGULIZI
Shule ni muunganiko wa madarasa tofauti tofauti katika ngazi na viwango tofauti tofauti yenye lengo la kumfundisha mtu mtu kujua jambo, au mambo fulani au kitu fulani kwa kina na weledi sana. Na katika shule kuna vipimo au mitiani toka darasa hadi darasa ambavyo hutumika kumpima mtu kama amejua na kufahamu jambo fulani na kwamba anastahili kuvuka na kwenda ngazi au kiwango cha juu zaidi kwa kuingia darasa linalofundisha viwango hivyo vya elimu au mafundisho.
Lengo ni mwanafunzi afikie kiwango fulani cha kujua jambo fulani kitakachomsaidia kuishi maisha yake kwa ufahamu na ujuzi aliona juu ya jambo lile akikabiliana na changamoto za kimaisha anazokuta nazo siku kwa siku.
Mungu anayoshule katika maisha yetu, na lengo la shule hiyo ni kutufundisha tumjue yeye katika kimo, kina, mapana na marefu, na anazo njia mbalimbali za kutufundisha anazotumi. Yeye mwenyewe ndiye mwalimu mkuu katika shule yake, na anatufundisha kumjua yeye kupitia mambo mbalimbali anayofanya katika maisha yetu siku kwa siku.
Zaburi 32:8
- Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, Nitakushauri, jicho langu likikutazama
Katika mstari huu mambo manne yametajwa, ambayo anayo mwalimu katika shule yake. Mungu ndiye mwalimu katika shule yake maishani mwetu, na kila siku kuna darasa na kipindi ambacho kwacho anafanya mambo manne hayo yaliyosemwa katika mstari huo.
- Jambo la Kwanza: NITAKUFUNDISHA
Jambo la kwanza ambalo kila siku Mungu analifanya katika maisha yako, ni kukufundisha wewe, hii maana yake kila katika siku moja kuna hatua katika kumjua Yeye ambayo wewe kama mwanafunzi wake unapaswa kupiga, ili kuwe na tofauti ya jana na leo. Ili Mungu akufundishe, ni lazima akuingize darasani, na wewe pia ukubali kuingia darasani ili kufundishwa na yeye. Na hapa anazo njia nyingi ambazo atatumia kukufundisha wewe. Tutakapoendelea na somo letu tutazijua njia hizo ambazo Mungu anazitumia kila siku kutufundisha.
Ili Mungu akufundishe anapokuingiza darasani, anahitaji ufahamu wako. Anapotaka kukufundisha kitu cha kwanza atakachokuwa anahitaji ni kuupata ufahamu wako. Hawaze kukufundisha chochote kama hajaupata ufahamu wako na wewe hujampa ufahamu wako.
Ili mtu aweze kujifunza na kuelewa jambo anahitaji kuuelekeza (to apply) ufahamu wake kwanza kwa mwalimu wake, na pili katika kile ambacho mwalimu wake anataka kumfundisha. Na ili mwalimu aweze kufanikiwa kuingiza funzo kwa mwanafunzi wake, ni lazima kwanza apate ufahamu wa mwanafunzi wake. Pasipo ufahamu wa mwanafunzi mwalimu hawezi kumfundisha mwanafunzi na wala mwanafunzi hawezi kujifunza jambo toka kwa mwalimu wake.
Kila siku ni siku ya kujifunza kwa sababu kila siku ni siku ya wewe kukua na kuongezeka kiufahamu katika kumjua Mungu. Na kila siku iwe hujaenda kanisani au umeenda, uwe kazini au popote pale, kuna kitu Mungu amekusudia wewe ujifunze ili ukue katika kumjua yeye, usibaki kuwa mchanga katika ufahamu wako.
Je, jana ulijifunza nini, na leo umejifunza nini kinachoongeza ujuzi wako katika kumjua Mungu? Kwa kiwango unachomjua, kwa kiwango icho hicho atajidhihirisha kwako, na kwa kwa kadiri unavyomjua ndivyo unavyozidi kuwa karibu naye, na unavyozidi kuwa karibu naye ndivyo unavyomjua zaidi, na unavyomjua zaidi ndivyo unavyomwamini zaidi, na unavyomwamini zaidi ndivyo anavyojidhihirisha maishani mwako kwa kazi zake anazofanya maishani mwako.
- Jambo la Pili: NA KUKUONYESHA_NJIA UTAKAYO IENDEA
Mungu anapokufundisha wewe kumjua yeye kwa njia yoyote ile, nawe ukamjua, jambo la pili atakalofanya, ni Kukuonyesha wewe njia utakayo iendea. Alipokuwa anakufundisha, alikuwa anacheza na ufahamu wako, katika kukuonyesha njia utakayoiendea, anahitaji moyo wako.
Kila siku kuna njia ambayo ni Mungu tu anaijua ambayo kupitia hiyo unaweza kufikia mafanikio katika maisha yao. Njia zipo nyingi, lakini njia iliyosawa na yenye mafanikio ya kweli ipo moja tu. Katika kitabu cha Mithali 16:25 Neno linasema,
“Iko njia ionekanayo kuwa ni sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.”
Njia ni nini? Njia ni namna ya kufanikisha jambo jema unalotaka au kulihitaji maishani mwako, ni namna ya kufanya ili kufikia makusudio au malengo yako. Ni kitu kinachotumika kukufikisha mahali unataka kwenda na kufika. Katika dunia hii njia nyingi katika mwanzo wake zina sura nzuri kiasi kwamba kwa akili zako huwezi kupambanua ni njia ipi ni njema na ina mwisho mzuri.
Tatizo sio mwanzo wa njia, tatizo ni mwisho wa njia. Usalama wa njia haupimwi katika mwanzo wake na wala mafanikio ya njia hayaonekani katika mwanzo wake bali katika mwisho wake. Na jambo baya kwa wanadamu wote, ni kwamba, hakuna mwanadamu aijuaye kesho yake ila Mungu pekee. Na kwa sababu hiyo, Mungu ndiye aijuaye njia salama ya wewe kuifikia kesho yako salama katika amani na mafanikio. Na ndio maana Biblia inasema kwamba,
“Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako” Mithali 3:5, 6
Kumtumaini Mungu ni kumwangalia yeye na kumtegemea yeye badala ya kuwaangalia watu, kujiangalia wewe mwenyewe, na kuyaangalia mazingira. Kumkiri Yeye katika njia zako zote ni kumwacha Yeye akuonyeshe njia kwa kumruhusu akuongoze. Watu wote wanaomkiri Mungu katika njia zao zote ni wale wanaosema kwamba, Mungu bila wewe siwezi, nenda mbele yangu uziongoze hatua zangu ili nisije nikapotea.
Umkabidhi Bwana njia yako, Pia umtumaini naye atafanya, Zaburi 37:5. Ukimkabidhi Mungu njia zako, atakuonyesha njia zake, na njia zake zitakupeleka katika majibu ya mambo unayoyatamani na kuyatazamia, maana atafanya hakika. Na ndio maana Mithali 16:3 anasema kwamba, Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatadhibitika.
Hili ni darasa kwa njia ya vitendo, Mungu kukuonyesha njia. Anakutoa Darasani anakuingiza shambani (field) katika uwanja wa utendaji.
- Jambo la Tatau:
NITAKUSHAURI
Mungu anapokuonyesha njia utakayoiendea, kitu kingine anachofanya wakati anakuonyesha njia utakayoiendea ni Kukushauri. Katika kukushauri, Mungu anahitaji mawazo yako, ili kupitia mawazo yako aseme na wewe moja kwa moja au kupitia Neno lake. Yeye ni mshauri wa ajabu, mwingi wa hekima, na hodari katika kazi zake, anayejua mwanzo wa neno na mwisho wa neno na kipi kitatokea katikati na yeye mwenyewe akiwa ndiye Mwanzo na ndiye Mwisho.
Anaposema kuwa “Nitakushauri” maana yake hatakulazimisha kufanya jambo kinyume cha hiyari na matakwa yako. Akiisha kukufundisha, akiisha kukuonyesha njia utakayoiendea, hawezi kukulazimisha katika kuenenda kwako, kitu atakachokuwa anafanya ndani yako kupitia mawazo yako ni kukushauri tu. Ni hiyari na utashi wako, kukubali au kukataa ushauri wake.
Hii kazi ya Mungu mwalimu, ni kazi anayoifanya katika shule yake maishani mwako, katika darasa la kimatendo, atakuwa hapo kukusimamia, akikufundisha, akikuonyesha njia utakayoiendea, lakini pia akikushauri mashauri ya ajabu.
- Jambo la Nne: JICHO_LANGU_LIKIKUTAZAMA
Ili kuhakikisha anafanya kazi yake ya uwalimu vizuri, hatakuacha peke yako, na wala hatakuwa pamoja na wewe lakini akiwa hakuangalii anafanya shughuli nyingine, anakuwa pamoja na wewe na jicho lake likikutazama vizuri sana ili aweze kukushauri vizuri, kukufundisha tena kwa kukumbusha pale uliposahau, kukusahihisha pale unapoanza kutoka nje ya njia aliyokuonyesha.
Ni mwalimu wa ajabu namna gani huyu ambaye wakati wote katika shule yake jicho lake lipo kwetu akitutazama, Yeye hasinzii, wala hachoki, wala halali kabisa, hata tunapokuwa tumelala, jicho lake linakuwa likitutizama.
Kila siku Mungu anakutazama, na kila siku kuna sauti ya Mungu moyoni mwako ikikuonyesha njia utakayoiendea, na kila siku anasikilizisha mawazo yake ndani yako akikushauri kitu cha kufanya na namna ya kukifanya vyema, na kila siku anajambo la kukufundisha ili umjue Yeye. Maisha yako yako ni shule ya Mungu anayoitumia kukufundisha kumjua yeye ili upate kufanikiwa katika njia zako zote.
"Bwana Mkombozi wako, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata. Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingelikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari. Tena wazao wako wangelikuwa kama mchanga, na hao waliotoka katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingelikatika, wala kufutwa mbele zangu." Isaya 48:17 – 19
Shule ya Mungu ni kwa faida yako mwenyewe na si kwa hasara. Mungu ni Mungu akufundishaye wewe ili uwe na faida, ni swala la wewe kuisikia sauti yake tu, na kukubali kuongozwa na Yeye katika njia ile anayokuonyesha.
Tutaendelea wakati ujao, Mungu akusaidie sana uelewe, kwa sababu ukiielewa kweli hii itafungua maisha yako katika kila eneo. Wiki hii tutakuwa tukiangalia kweli hii huku tukigusa kila eneo la maisha yetu kwa kuangalia mifano mingi katika Biblia. Kwa sababu ya urefu wa somo, nitakuwa naandika mambo mengi sana, naomba wewe ujitie nia katika kusoma yote, ukishindwa basi, ni kwa hasara yako mwenyewe.
Barikiwa.
Amen baba Kwa Somo zuri
ReplyDeleteKaribu kujifunza zaidi
DeleteAsante
DeleteUtukufu na heshima vina wewe wastahili Bwana wangu
ReplyDeleteAmen
ReplyDelete