YAJUE KUYATENDA MAPENZI YA MUNGU ILI KULETA THAMANI KWENYE MAISHA YAKO
…UTAIINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI… (Isaya 58:12)
Mafundisho ya Neno la Mungu
Na: Isaac Mwanzalila
Yeremia 29:11 ‘Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho’.
Tambua kwamba mawazo ya Mungu yanatuonyesha mapenzi yake kwetu na hivyo mawazo yake ndiyo mapenzi yake kwetu. Si watu wengi wanaojua kwamba kutokuyatenda mapenzi ya Mungu ni dhambi.
Yakobo 4:17 ‘Bali yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi’.
Ndio yeye mwenye kujua yaliyo mema (kilicho sahihi na au mapenzi ya Mungu) asiyatende kwake huyo ni dhambi.
Hebu tuone maandiko mbalimbali yanavyosema kuhusu jambo hili:
Yohana 5:30 ‘Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, KWA SABABU SIYATAFUTI MAPENZI YANGU MIMI, bali mapenzi yake aliyenipeleka’.
Hii ina maana BWANA Yesu alijifunza kutafuta kusikia kutoka kwa Mungu kwa kila jambo ambalo lilikuwa mbele yake ili apate kulitenda. Kusikia kwake ndiko kulimfanya afanye maamuzi ambayo ni sahihi mbele za Mungu tena ya haki hata kama mbele za wanadamu hayakuwa sahihi au hayakukubalika.
Daima BWANA Yesu hakutafuta mapenzi yake bali mapenzi ya Mungu kwenye kila jambo linalohusu maisha na huduma yake hapa duniani. Hii ina maana hata kama nafsi yake kuna mambo ilitaka alijizuia kwa kutafuta kujua kutoka kwa Mungu nini ni mapenzi makamilifu. Ndiyo alijua kwamba hakuja duniani kuishi kwa ajili yake bali kwa ajili ya yeye aliyempeleka yaana Baba.
Yohana 6:38 ‘Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili NIYAFANYE MAPENZI YANGU, bali mapenzi yake aliyenipeleka.
Lengo la andiko hili ni kutuonyesha kwamba hata Yesu naye alikuwa na mapenzi yake, lakini hakurusu mapenzi yake yachukue nafasi ya mapenzi ya baba hata kama kwake binafsi yalikuwa ni machungu (Mathayo 26:42). Basi nawe, tambua kwamba umeumbwa ili kuyatenda mapenzi ya Mungu kwenye maisha yako na si yako.
Waefeso 5:17 ‘Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana’. Ili kuyatenda mapenzi ya Mungu,
Ni jukumu la mwanadamu daima kutafuta kuyajua mapenzi ya Mungu kwenye kila eneo la maisha yake. Kutokujua mapenzi ya Mungu ni hatari na hupelekea watu wengi kuangamizwa na ndiyo maana imeandikwa ‘
Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa…’ (Hosea 4:6)
Je unajua nini yaliyo mapenzi ya Bwana kuhusu ndoa yako, watoto wako, elimu yako, huduma yako nk?
Kwa nini tutende Mapenzi ya Mungu?
Mathayo 6:10 ‘Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni’.
Mungu ni roho, bali mwanadamu amepewa mwili wa damu na nyama na hivyo kuwekwa aimiliki na kuitawala dunia. Kutokea kwenye ulimwengu wa roho, Mungu amekusudia watoto wake wahakikishe mapenzi yake yanatimizwa hapa duniani, naam unaishi ili kuyatenda mapenzi ya Mungu na si vinginevyo.
Waefeso 5:5, 9 & 11 ule mstari wa 11 ‘Na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake’.
Ni ajabu sana kwamba kumbe katika kufanya kazi zake, Mungu huzingatia shauri/kusudi la mapenzi yake (yeye Mungu anataka nini). Ndio mapenzi ya Mungu yamejaa makusudi yake, na yeye huyazingatia hayo katika utendaji wake.
Je, umeona siri hii? Kilichomfanya atuchague ni kusudi lake yeye, na tena yeye hufanya mambo yake yote kwa shauri la mapenzi yake. Hii ina maana kwa kila hatua, ngazi ya maisha ya watoto wake, Mungu huruhusu au hufanya mambo yatokee kwa kuzingatia mahitaji ya mapenzi au kusudi lake, naam mapenzi yake ndiyo humuongoza katika kufanya mapenzi yake na si vinginevyo. Hii ni kutuambia ni lazima kuwa makini sana na kuhakikisha unaruhusu mapenzi ya Mungu kuhusu nini unasomea, wapi unasoma, wapi unaishi, nani anakuwa mwenza wako nk.
1 Yohana 2:17 ‘Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele’.
Andiko hili linatufundisha yafuatayo:
1.Kwamba, Yesu alijua ameletwa duniani ili kuyatenda mapenzi ya baba yake na hivyo mosi alihakikisha anatafuta kujua yapi ni mapenzi ya baba yake kwa kila hatua, majira au wakati na pili aliyapa kipaumbele cha pekee mapenzi ya baba yake kuzidi chakula, furaha yake ilikuwa ni kuona amekamilisha lengo au kile ambacho alitakiwa kufanya kwa majira husika.
2.Kwamba, mapenzi ya Mungu yamebeba kusudi la Mungu na kadri mtu anavyoyatenda mapenzi ya Mungu (kazi za kila siku, wiki, mwezi nk) NDIVYO anavyolitekeleza kusudi la Mungu na kulitimiza maishani mwake.
3.Kwamba, Kusudi la Mungu limefungwa kwenye muda, hivyo kadri mtu anavyozitenda kazi zilizofungwa kwenye kusudi hilo ndivyo majira ya hilo kusudi yanavyotoa ushirikiano kwa mtu husika.
4.Kwamba, Yesu alijua yupo duniani kwa ajili ya kusudi la baba yake, kwa hiyo licha ya kutambua kusudi, alimtambua kwanza mwenye kusudi, akamheshimu na akakubali kukaa chini ya uongozi wake.
Mungu anataka watoto wake aliowaita kukamilisha kazi ile ambayo amewaitia, na kwamba ni muhimu kwao kujua majukumu yao na kuyatenda. Mungu anatafuta mtu atakayekuwa tayari kujizuia kuyatenda mapenzi yake binafsi na kudumu kuyatenda mapenzi ya Mungu (asomaye n afahamu).
Kwa ufupi, mapenzi ya Mungu ni wema, ukamilifu na upendo (Warumi 12:2).
ReplyDelete