YATAZAME MAMBO KUTOKA KWENYE ULIMWENGU WA KIROHO ILI UFANIKIWE

... UTAINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI...(ISAIAH 58:12) 



…UTAIINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI… (Isaya 58:12)

Mafundisho ya Neno la Mungu…UTAIINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI… (Isaya 58:12) Mafundisho ya Neno la Mungu

Na: Isaac Mwanzalila 


Katika 2 Wafalme 6:15-17 imeandikwa ‘Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje? Akamjibu, USIOGOPE; maana WALIO PAMOJA NASI ni wengi kuliko wale walio pamoja nao. Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote’.


Kuna tofauti kubwa sana ya kuyatazama mambo kwa macho ya mwili na kuyatazama kwa macho ya kiroho. Ndio, ipo tofauti ya kuona mambo kutokea kwenye ufalme wa nuru na kuyaona kutokea kwenye ufalme wa giza. Tambua kuwa kila hatua au changamoto unayoipitia, namna ulimwengu wa roho wanavyoitazama ni tofauti na ulimwengu wa mwili wanavyoitazama. Hivyo basi watoto wa Mungu wanapaswa wajifunze kuyatazama mambo kutokea kwenye ulimwengu wa roho kwa macho ya ufalme wa nuru ili wafanikiwe.

Je, Ulimwengu wa roho ni nini?


Biblia kwenye kitabu cha Waefeso 1:3 na Waefeso 6:10-12 imeeleza kuhusu uwepo na uhalisia wa ulimwengu wa roho kama ilivyo kw ahabari ya ulimwengu wa mwili. Ulimwengu wa roho ni makazi ya ufalme wa Mungu na ufalme wa Shetani, kila ufalme ukiwa na eneo lake la utawala ingawa Mungu au viumbe wa ufalme wa nuru wana uwezo wa kuingia na kutoka eneo la ufalme wa giza ikiwa kuna kusudi la kwenda huko.
Ulimwengu wa roho ni makazi ya roho zisizo na mwili wa damu na nyama na huko kuna viumbe mbalimbali vya kila ufalme ambapo Malaika ndio watendaji wakuu kwenye ufalme wa nuru na Mapepo ndio watendaji wakuu kwenye ufalme wa giza. Falme hizi mbili zinafanya kazi kwenye ulimwengu wa mwili kutokea kwenye ulimwengu wa roho, kwa sababu wao ni roho zisizo na mwili huu wa damu na nyama (Yohana 4:24 na Waefeso 2:2).
Kuona mambo kwa jicho la ufalme wa nuru kunamsaidia mtu kunena, kutenda au kufanya maamuzi. Hii ina maana kadri mtu anavyoongeza uwezo wake wa kuona ndivyo anavyojiweka kwenye nafasi nzuri ya kufanya maamuzi sahihi. Ndio maana vita kubwa inayopigwa na ufalme wa giza dhidi ya Watoto wa Mungu ni kuwazuia wasione mambo kutokea kwenye ulimwengu wa roho kwa jicho la ufalme wa nuru.

Kwa nini kuyatazama mambo kutokea kwenye ulimwengu wa roho?


• Neno la Mungu ndio sheria inayotawala kwenye ulimwengu wa roho. Neno ndio linaloufungua na kuufunua ulimwengu wa roho kwenye roho ya mtu. Hivyo ni wajibu wa mtu kulisoma na kulitafakari neno kila siku ili kuona kilichomo ndani yake. Ndio, Mungu anatatarajia watoto wake waweze kuona mambo kwa kulisoma neno lake, naam wasome na kuwaza mpaka waone kilichobebwa kwenye neno (Yeremia 1:11-12, Warumi 8:1-2, Mathayo 7:21-23, Ufunuo wa Yohana 12:17).
• Matokeo na uhalisia wa jambo kwenye ulimwengu wa mwili unaanzia na unategemea utendaji wa mtu kwenye ulimwengu wa roho. Chochote kinachotokea duniani kimefanyika kwanza kwenye ulimwengu wa roho. Maamuzi anayofanya mtu kwenye ulimwengu wa roho ndio yanayoamua hali na hatma yake kwenye ulimwengu wa mwili. Tambua, watoto wa Mungu wana mamlaka ya kuamua namna wanavyotaka mambo yawe kwenye ulimwengu wa mwili kwa kutumia nafasi zao za ulimwengu wa roho. Rejea Isaya 62:-7, 1 Wakorintho 2:8-9. (Isaya 62:6-7, Danieli 4:13-17, Danieli 10:11-13, 2Wakorintho 10:3-5).


• Kuona ndio msingi wa kufanikiwa katika kuvipga vita vya kiroho – Kuyatazama mambo kutokea kwenye ulimwengu wa roho ni moja ya mbinu za kumsaidia mwamini katika kuvipiga vita vya kiroho na kushinda. Kushindwa au anguko la wakristo wengi leo ni matokeo ya kutokujua namna ya kuvipiga vita vya kiroho. Hivyo kuwa na uwezo wa kuona mambo kutokea kwenye ulimwengu wa roho ni muhimu sana na tena ufunguo wa ushindi (2 Wafalme 6:8-11).
Kupitia ujumbe natamani ujifunze na kujua mambo yafuatayo:
  1. Moja, katika kila hali au changamoto unayoipitia, mtazamo wa ulimwengu wa roho, juu ya jambo hilo ni tofauti na wanadamu kwenye ulimwengu wa mwili wanavyolitazama. Wakati wanadamu na dunia vinajaribu kukuonyesha na kukuthibitishia kwamba wewe ni wa kufeli, Mungu anakuhakikisha kwamba anayo mawazo ya amani juu yako. Ndio, wakati Mungu anataka watoto wake wayatazame mambo kutokea kwenye ulimwengu wa roho, Shetani anataka watu wayatazame mambo kutokea kwenye ulimwengu wa mwili. Hivyo basi hakikisha kwamba daima unajifunza kuyatazama mambo kutokea kwa jicho la ufalme wa nuru kupitia neno la Mungu.
  2. Mbili, pale tunapoyatazama mambo kutokea kwenye ulimwengu wa roho ndipo tunapoweza kuyaona na kuyatambua mawazo ya Mungu juu yetu na hivyo kuwa na furaha, amani hata katika mazingira ambayo adui zetu zetu walitarajia tufeli, tuumizwe na nyuso zetu zijae fedheha na aibu (Rejea Isaya 55:8–9 na 1 Wakorintho 2:9-10)
  3. Tatu, kwa Mungu yako mambo yanayokuhusu wewe, ambayo hakuna jicho limeyaona, wala sikio lililoyasikia na tena hayajaingia katika moyo wa mwanadamu yeyote maana ni mahususi kwa ajili yako. Jukumu lako ni kujifunza kutazama kila hatua unayopitia au kukutana nayo maishani mwako kwa jicho la neno la Mungu. Ukifanya hivyo mawazo hayo yatafunuliwa kwako nawe utajua fikra za ufalme wa nuru kuhusu jambo hilo. Naam kadri unavyotii kutenda yale unayoona ndivyo unavyofanikiwa, kuwa salama na thamani yako kuongezeka kwenye ufalme wa nuru.
  4. Nne, Neno la Mungu linafunua kwetu, linatujulisha naam linatuonyesha namna ya kufanya mambo. Hivyo, ikiwa tutalipa nafasi litawale na kuyaongoza maisha yetu, neno litatusaidia, mosi kututoa kwenye fikra, mitazamo na makusudi yetu mabaya, pili litatuongoza katika njia sahihi ya kufanya maamuzi na mwisho tutaweza kushinda fikra na maamuzi yoyote yailiyo kinyume na mapenzi ya Mungu kwenye maisha yetu.


Neno la Mungu pekee, ndiyo limepewa heshima hiyo na kwamba Mungu mwenyewe, amelikuza neno lake, kuliko jina lake. Hii yote ni kutuonyesha umuhimu na thamani ya neno lake kwenye maisha yetu. Hivyo, kama huna ndihamu ya kuwa na muda wa kusoma na kutafakari neno la Mungu ujue umechagua kufeli kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yako (Yohana 1:1-3,14, Waebrania 4:12, Zaburi 138:2)
Hitimisho: Mpenzi msomaji, je, wewe unaona mambo kwa macho yapi? Macho ya ufalme wa nuru, ufalme wa giza au ya mwili? Ujasiri wa Elisha kumweleza Mtumishi wake USIOGOPE ulichangiwa na yeye KUONA kwenye ulimwengu wa roho kile ambacho Msaidizi wake hakukiona maana aliona jeshi la BWANA lenye nguvu kushinda la adui zao waliowazingira kwenye ulimwengu wa mwili.
Haijalishi hali unayoipitia sasa ni ya kukatisha tamaa au kuvunja moyo kwa kiwango gani, jambo unalopaswa kufanya ni kuitazama au kulitazama jambo hilo kutokea kwenye ulimwengu wa roho kwa jicho la ufalme wa nuru kupitia neno la Mungu. Ukifanya hivyo ndipo macho yako yatafumbuka nawe utagundua kwamba hakuna neno au jambo lolote lenye nguvu kumshinda Yesu, bali ni jukumu lako kuamini kile kilichoelekezwa kwenye neno la Mungu ili uwe upande wa washindi.


Uwezo wa kuona mambo kutokea kwenye ulimwengu wa roho ni jambo muhimu na la lazima kwa kila mwamini. Basi mosi hakikisha unatunza macho yako ya kiroho ili yasipoteze uwezo wako wa kuona, vinginevyo utadumbukia shimoni. Pili, hakikisha unaongeza uwezo wako wa kuona kwenye ulimwengu wa roho na mwisho dumu kuyatazama mambo kutokea kwenye ulimwengu wa roho ili kuyatenda mapenzi ya Mungu na hivyo kufanikiwa.

Utukufu na Heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA wangu.


Comments

Popular posts from this blog

ONGEZA UFAHAMU WAKO KUHUSU NDOTO ILI IKUSAIDIE KUFANYA MAAMUZI SAHIHI (SEHEMU ya PILI)

MAMBO YA KUMSAIDIA KIJANA ALIYEOKOKA AISHI MAISHA YENYE USHUHUDA MZURI

SHULE YA MUNGU MAISHANI MWAKO.